By:Hassan Pojjo

WADAU wa soka katika Kaunti ya Mombasa wamekaribisha uamuzi wa Mahakama ya Michezo nchini (SDT) wa kuthibitisha uhalali wa kanuni za Shirikisho la Soka Kenya (FKF) kuhusu mfumo wa kupanda na kushuka daraja kwa mwaka 2025.
Uamuzi huo umeeleza kuwa kanuni hizo ziliidhinishwa kihalali na Kamati Kuu ya FKF (NEC) na kwamba hazikuhitaji kuwasilishwa kwa ajili ya kupitishwa na Mkutano Mkuu wa Shirikisho hilo.
Akizungumza baada ya uamuzi huo, Mwenyekiti wa FKF Mombasa, Alamin Ahmed Abdalla, amesema uamuzi huo ni hatua muhimu katika kuimarisha uwazi na utawala bora ndani ya FKF.
Alamin amesema wadau wa soka wanapaswa kuheshimu uamuzi wa chombo cha kisheria na sasa nguvu zielekezwe katika maendeleo ya soka badala ya kuendeleza mvutano kuhusu kanuni hizo.
Amesema uamuzi huo unatoa mwanga kuhusu mamlaka ya NEC katika kutunga na kuidhinisha kanuni zinazohusu uendeshaji wa mashindano, ikiwemo mfumo wa kupanda na kushuka kwa madaraja.
Mwenyekiti huyo ametoa wito kwa pande zote zilizokuwa zikihusika katika mzozo huo kukubali uamuzi wa SDT na kuhakikisha suala hilo linafikia tamati.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa viongozi wa soka kuweka mbele maslahi ya wachezaji, vilabu na mashabiki, akisema utulivu wa kiutawala ni muhimu kwa maendeleo ya soka nchini.
Uamuzi huo unatarajiwa kutoa mwelekeo mpya katika utekelezaji wa mfumo wa madaraja ya soka, huku wadau wakisubiri kuona namna kanuni hizo zitakavyotekelezwa katika mashindano ya msimu unaofuata.
Wadau wa soka Mombasa sasa wanatarajia mzozo huo kufungwa rasmi ili vilabu na viongozi wa soka waweze kuelekeza nguvu zao katika maandalizi ya msimu mpya na kuinua kiwango cha soka katika eneo la Pwani.
