By:Hassan Pojjo

Mwenyekiti wa Shirikisho la Soka Kenya (FKF) Tawi la Kaunti ya Mombasa, Alamin Mohammed, amezindua rasmi Ligi ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 13 na 17, katika juhudi za kuibua na kukuza vipaji vya soka vilivyoko mashinani.
Ligi hiyo inalenga kuwapa vijana wenye vipaji fursa ya kucheza, kuonyesha uwezo wao na kutambulika na makocha pamoja na viongozi wa soka, hatua inayoweza kuwawezesha kupata nafasi katika timu kubwa siku zijazo.

Akizungumza katika uwanja wa Bombolulu Workshop wakati wa uzinduzi wa ligi hiyo, Alamin alisema FKF Mombasa imeamua kuanzisha mashindano hayo baada ya kubaini kuwa vipaji vingi vya vijana vinapotea kutokana na ukosefu wa majukwaa ya kuwawezesha kuonyesha uwezo wao.
“Kama ofisi ya Shirikisho Mombasa tumeona jinsi vipaji vya watoto wetu wachezaji vinavyopotea na vilevile kutopata nafasi nzuri ya kucheza na kuonekana. Ndiposa tukaleta ligi hii, hasa wakati huu wa likizo fupi ambapo wanafunzi wengi wapo majumbani,” alisema Alamin.

Alamin alisema ligi hiyo pia ni sehemu ya juhudi za FKF Mombasa kuhakikisha vijana wanatumia muda wao vizuri kupitia michezo, badala ya kujihusisha na shughuli zinazoweza kuhatarisha maisha na mustakabali wao.
Aidha, aliwataka vijana kuwa makini na matumizi ya dawa za kulevya, akieleza kuwa uraibu wa dawa za kulevya ni miongoni mwa changamoto zinazowakabili vijana wengi katika maeneo mbalimbali ya Mombasa.
Mwenyekiti huyo alisema michezo, hususan soka, inaweza kuwa nyenzo muhimu ya kuwaweka vijana katika mazingira salama na kuwapa mwelekeo mzuri wa maisha kupitia vipaji vyao.

Alamin pia aliwapongeza wadau walioshirikiana na FKF Mombasa kufanikisha ligi hiyo, akiwataja Mohammar Jaffar Foundation na Serani kwa mchango wao wa kufadhili mashindano hayo.

Alisema ushirikiano kati ya FKF, wafadhili, wazazi, makocha na wadau wengine wa michezo ni muhimu katika kuhakikisha vipaji vya vijana vinatambuliwa na kuendelezwa tangu wakiwa katika umri mdogo.
Ligi hiyo inatarajiwa kuwa jukwaa muhimu kwa vijana wa Mombasa kuonyesha vipaji vyao, huku FKF Mombasa ikilenga kuendeleza mfumo wa kutambua vipaji vipya na kuwaandaa wachezaji kwa ajili ya kushiriki katika viwango vya juu vya soka nchini.
