Share this to

By:Alii Vincent

Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki amewasili jijini Dar es Salaam, Tanzania, kumwakilisha Rais Dkt. William Ruto katika Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Shirika la Africa50 na Jukwaa la Miundombinu Barani Afrika (Infra for Africa Forum), unaowakutanisha viongozi wa serikali, taasisi za kifedha na wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali.

Mkutano huo unalenga kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika kufadhili na kuharakisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya miundombinu barani Afrika, hususan katika sekta za usafiri, nishati, teknolojia ya kidijitali na maendeleo ya miji.

Kupitia taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Naibu Rais, Prof. Kindiki anatarajiwa kuwasilisha msimamo wa Kenya kuhusu umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi ili kuongeza uwekezaji katika miradi ya maendeleo yenye mchango mkubwa kwa ukuaji wa uchumi.

Serikali ya Kenya imeendelea kutangaza uwekezaji wa miundombinu kuwa nguzo muhimu ya ajenda yake ya maendeleo, ikieleza kuwa uboreshaji wa miundombinu utachochea biashara, kuongeza ushindani wa uchumi na kuimarisha muunganiko wa masoko ya kikanda.

Ushiriki wa Kenya katika mkutano huo unatarajiwa kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na taasisi za kimataifa za ufadhili, pamoja na kufungua fursa mpya za uwekezaji zitakazochangia maendeleo ya Kenya na bara la Afrika kwa ujumla.


Share this to

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *