By:Hassan Pojjo

Wakaazi wa Majengo/Mwembetayari katika eneo bunge la Mvita wanatarajia kunufaika na ujenzi wa Barabara ya Burnley Access Road, unaoendelea kwa kasi na unaolenga kuboresha usafiri pamoja na kuchochea shughuli za kiuchumi katika eneo hilo.
Mradi huo wa uwekaji wa mawe ya cabro unatarajiwa kurahisisha usafiri wa kila siku kwa wakazi, wafanyabiashara na wanafunzi, huku ukiondoa changamoto zilizokuwa zikisababishwa na ubovu wa barabara, hasa wakati wa mvua.

Mbunge wa Mvita, Mohammed Masoud Machele, amesema mradi huo ni sehemu ya juhudi za kuboresha miundombinu na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora katika maeneo ya makazi na biashara.
Ameeleza kuwa maendeleo ya miundombinu ni msingi muhimu wa kukuza uchumi wa eneo bunge la Mvita, akibainisha kuwa serikali inaendelea kutekeleza miradi yenye manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi ili kuboresha maisha yao na kuongeza fursa za biashara.

Wakazi wa eneo hilo wameeleza matumaini yao kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutaboresha mazingira ya biashara, kuongeza usalama wa watumiaji wa barabara na kuinua hadhi ya Majengo/Mwembetayari kupitia miundombinu ya kisasa.

Burnley Access Road ni miongoni mwa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Mvita kwa lengo la kuboresha huduma za usafiri, kuimarisha mazingira ya uwekezaji na kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Mbunge Machele ameahidi kuendelea kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yote ya Mvita ili kuhakikisha wananchi wananufaika na huduma bora chini ya kaulimbiu yake ya “Huduma na Maendeleo.”
