By:Farida Ali

Hali ya taharuki ilitanda katika Kisiwa cha Lamu, Kaunti ya Lamu, baada ya afisa mmoja wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kujeruhiwa na kijana.
Tukio hilo limeibua wasiwasi mkubwa miongoni mwa wakazi wa eneo hilo, huku wanaharakati na viongozi wa jamii wakilaani vikali kitendo hicho na kutaka hatua za haraka zichukuliwe ili kuimarisha usalama.
Wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Vocal Africa, Hussen Khalid, wanaharakati hao wamesema matukio ya ukosefu wa usalama yanayowahusisha vijana yamekuwa yakiongezeka katika Kaunti ya Lamu.
Wameitaka Idara ya Usalama kuimarisha operesheni zake na kushughulikia changamoto hiyo kwa haraka.
Aidha, wanaharakati hao wamewataka wananchi kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa muhimu zitakazosaidia katika uchunguzi wa tukio hilo na kuzuia matukio mengine ya uhalifu.
