Share this to

By:Hassan Pojjo & Alii Vincent

Kenya imeweka historia mpya katika juhudi za uhifadhi wa mazingira baada ya kupanda miche ya mikoko 4,124 ndani ya sekunde 15 na kufanikiwa kuvunja Rekodi ya Dunia ya Guinness katika hafla iliyofanyika katika mfumo wa ikolojia wa mikoko wa Jomvu Kuu, Kaunti ya Mombasa.

Zoezi hilo lililoandaliwa na kuongozwa kwa ushirikiano kati ya Idara ya Misitu nchini (KFS), Chama cha Skauti Kenya (KSA) na Wakfu wa M-PESA Foundation, liliwaleta pamoja maelfu ya washiriki wakiwemo wanafunzi wa skauti kutoka shule mbalimbali za ukanda wa pwani, wanajamii, viongozi na wadau wa mazingira. Hafla hiyo ilikuwa sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kuhifadhi Mfumo wa Ikolojia wa Mikoko.

Ili kutimiza vigezo vya Rekodi za Dunia za Guinness, shughuli hiyo ilisimamiwa kwa umakini mkubwa, huku maafisa 50 wa KFS wakihakikisha nidhamu na utekelezaji sahihi wa zoezi hilo, pamoja na uwepo wa mashahidi wawili rasmi na huru waliokuwa wakifuatilia kila hatua ya mchakato huo.

Akizungumza baada ya kufanikiwa kwa rekodi hiyo, Naibu Mkuu wa Misitu nchini, Dkt. Clement Ng’oriareng’, aliwapongeza washiriki kwa nidhamu, kujitolea na uzalendo wao katika kulinda mazingira.

Hafla hiyo pia iliwakutanisha wanaharakati wa mazingira pamoja na washikilizi wa rekodi za Guinness, akiwemo Truphena Muthoni ambaye aliweka rekodi ya kuukumbatia mti kwa saa 72 mfululizo, na Jimmy Cowel aliyepanda miti 32,000 ndani ya saa 24.

Mbunge wa Jomvu, Badi Twalib, aliungana na viongozi mbalimbali wa Kaunti ya Mombasa, wanachama wa Kenya Scouts Association, M-PESA Foundation na wananchi katika shughuli hiyo ya kihistoria iliyofanyika katika eneo la Kwa Fara Village, Jomvu Kuu.

Akihutubia washiriki, Badi Twalib alisema kuwa zoezi hilo halikuwa tu jaribio la kuvunja rekodi ya dunia, bali lilikuwa ishara ya dhamira ya pamoja ya kulinda mazingira, kurejesha uoto wa asili wa ukanda wa pwani na kuhakikisha vizazi vijavyo vinapata mazingira salama na yenye afya.

Alisisitiza kuwa mikoko ina mchango mkubwa katika kupunguza hewa ya ukaa, kuhifadhi viumbe hai, kuzuia mmomonyoko wa ardhi na kulinda mfumo wa ikolojia wa maeneo ya pwani unaokabiliwa na athari za shughuli za kibinadamu na mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake, Caren Basiye, Afisa wa Safaricom anayehusika na maendeleo ya biashara na shughuli za kijamii kupitia Wakfu wa M-PESA, alisema ushiriki wa taasisi hiyo unaonyesha dhamira ya sekta binafsi katika kuunga mkono juhudi endelevu za uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Viongozi wa Kaunti ya Mombasa, akiwemo Waziri wa Kamati ya Utendaji ya Kaunti anayesimamia mazingira Mohamed Osman Ali na MCA wa Jomvu Kuu Joshua Ong’au Mose, walitoa wito kwa wananchi kuendeleza utamaduni wa kupanda na kutunza miti kila siku badala ya kusubiri kampeni maalum za mazingira.

Washiriki walihitimisha hafla hiyo kwa kuahidi kuendelea kushiriki katika shughuli za uhifadhi wa mazingira, huku viongozi wakisisitiza kuwa kupitia ushirikiano wa serikali, sekta binafsi, mashirika ya kijamii na wananchi, inawezekana kuijenga Mombasa iliyo safi, ya kijani na yenye uwezo mkubwa wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mafanikio hayo yanaifanya Kenya kuwa miongoni mwa mataifa yanayoonyesha mfano wa jinsi hatua za pamoja za jamii zinavyoweza kuleta matokeo makubwa katika mapambano ya kimataifa dhidi ya uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi.


Share this to

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *