By:Alii Vincent

Gavana wa Kaunti ya Mombasa Abdulswamad Sharif Nassir amewataka wakaazi wa Mombasa na eneo la Pwani kwa ujumla kukataa siasa za ukabila, chuki na mgawanyiko.
Akizungumza katika eneo la Kibarani, Kaunti Ndogo ya Jomvu, Gavana Nassir amewakosoa viongozi wanaotumia siasa za utengano, akisema hawana sera wala dhamira ya kuleta maendeleo kwa wananchi wa Pwani.
Badala yake, Gavana Nassir amewahimiza wakaazi kushirikiana na serikali ya Rais William Ruto ili kuhakikisha eneo hilo linanufaika na miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali.
Kauli hiyo imeungwa mkono na Mbunge wa Jomvu Badi Twalib, ambaye amesema ushirikiano kati ya viongozi wa kitaifa na wa eneo hilo umeanza kuleta matokeo, ikiwemo zoezi la upimaji wa ardhi baada ya serikali kununua mashamba kutoka kwa wenye mashamba makubwa na kuyagawa kwa wananchi waliokuwa wakiishi kama maskwota. Viongozi hao walikuwa wakizungumza wakati wa uzinduzi wa jengo la walimu katika Shule ya Kibarani, pamoja na uzinduzi wa ujenzi wa barabara ya Kibarani Ring Road.
