Share this to

Rais William Ruto pamoja na Mawaziri wa Baraza la Mawaziri wamefanya mabadiliko makubwa katika uongozi wa mashirika mbalimbali ya umma, kupitia uteuzi na uteuzi upya wa wenyeviti na wajumbe wa bodi.

Mabadiliko hayo yamechapishwa kwenye Gazeti Rasmi la Serikali la Julai 24, 2026, na yanahusu sekta muhimu zikiwemo nishati, kilimo, afya, elimu, maji, biashara, mawasiliano, kazi na utawala wa umma.

Miongoni mwa walioteuliwa upya na Rais Ruto ni Mhandisi Gilbert Maluki ambaye ataendelea kuhudumu kama Mwenyekiti asiye mtendaji wa Bodi ya Mamlaka ya Umwagiliaji kwa kipindi kingine cha miaka mitatu.

Rais pia amemteua Moses Wekesa Mwambu Mabonga kuwa Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Mamlaka ya Kudhibiti Nishati na Petroli (EPRA), huku akifuta uteuzi wa awali uliofanywa mwaka 2025.

Katika mabadiliko hayo, uteuzi wa Daktari Thuo Mathenge kama Mwenyekiti wa Shirika la Utafiti wa Kilimo na Mifugo nchini (KALRO) umebatilishwa.

Waziri wa Hazina ya Taifa John Mbadi amemteua upya George Murugu Muthui kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Rufaa ya Ununuzi wa Umma, pamoja na kuwateua upya wajumbe watano kwa muhula wa miaka mitatu. Aidha, Johnson Osoi ameendelea kuhudumu kama Mwenyekiti wa Bodi ya Local Authorities Provident Fund.

Katika Wizara ya Mambo ya Ndani, Waziri Kipchumba Murkomen amemteua Adan Haji Ali kuwa Mwenyekiti wa Mamlaka ya Kusimamia Mashirika ya Kijamii (PBO Authority), huku Sophie Chepkorir Sang akiteuliwa kuwa mjumbe wa bodi ya NACADA.

Sekta ya afya pia imeguswa, ambapo Waziri Aden Duale ameongeza muda wa kuhudumu kwa wakurugenzi watatu wa Bodi ya KEMSA.

Kwa upande wa elimu, Waziri Julius Ogamba amefanya uteuzi na uteuzi upya katika mabaraza ya vyuo vikuu na taasisi za kitaifa za mafunzo ya ufundi.

Katika Wizara ya Maji, Daktari Njage Makanga ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Wakala wa Maendeleo ya Miradi ya Maji wa Bonde la Central Rift Valley, akichukua nafasi ya Samuel Mathenge Nderitu.

Mawaziri wengine akiwemo Alfred Mutua wa Kazi, Lee Kinyanjui wa Biashara, Mutahi Kagwe wa Kilimo, Deborah Barasa wa Mazingira na William Kabogo wa ICT pia wamefanya uteuzi mbalimbali katika mashirika yaliyo chini ya wizara zao.

Kwa ujumla, wengi wa walioteuliwa na walioteuliwa upya wanatarajiwa kuhudumu kwa kipindi cha miaka mitatu.


Share this to

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *