By:Robert Mutasi

Rais William Ruto ametangaza kuwa serikali yake itaanzisha mfumo mpya wa ufadhili utakaohakikisha wanafunzi wote waliopangwa kujiunga na vyuo vikuu na vyuo vya mafunzo ya ufundi wanapata elimu bila kikwazo cha kifedha.
Ruto, aliyekuwa akizungumza na wakazi wa Nairobi, alisema elimu ndiyo msingi wa usawa nchini na serikali yake imeipa kipaumbele kwenye bajeti ya taifa.
“Elimu ndio inatupatia usawa kama taifa. Na ndio sababu nimeweka pesa nyingi kwa mambo ya elimu kwa bajeti yetu,” alisema Ruto.
Rais alisema serikali tayari imeajiri walimu, imefanya mabadiliko kwenye mtaala na kujenga madarasa kama sehemu ya kuimarisha sekta ya elimu.
Alitetea mfumo wake tata wa ufadhili wa vyuo vikuu uliozinduliwa mwaka 2023, akisema uliokoa vyuo vikuu vya umma vilivyokuwa ukingoni mwa kufungwa.
“Tulitoa pale nyuma 2022 ma-universities walikuwa wanafunga, hawakuweza kulipa walimu, hawakuweza kulipa suppliers, hata mshahara ya wale lecturers haikuwa inatosha. Nikabadilisha tukatengeneza model mpya. Hiyo model imebadilisha mambo katika ma-university,” alisema.
Ruto alisema sasa serikali inapeleka mfumo huo hatua moja mbele ili kuhakikisha kila mwanafunzi anapata ufadhili.
“Mimi nimesema sasa tunapeleka hiyo model one more step forward,” alisema.
Alifichua kuwa Mswada wa Marekebisho wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, HELB, upo bungeni sasa, ambao utaweka msingi wa kisheria wa kuhakikisha kila mtoto wa Kenya aliyewekwa chuoni anafadhiliwa kikamilifu.
“Iko sheria bunge saa hizi ya Higher Education Loans Board Amendment Bill ambayo sasa itatuwezesha kuhakikisha ya kwamba kila mtoto wa Kenya ambaye amekuwa placed kwa TVET ama university tutahakikisha ya kwamba kuna funding ama kuna pesa ya kusomesha watoto wetu wote,” alisema.
Akilinganisha na sera ya elimu ya msingi ya bure ya Rais wa tatu Mwai Kibaki, Ruto alisema wakosoaji waliidhihaki awali lakini baadaye ilibadilisha taifa.
“Unajua wakati rais wa tatu wa Kenya mheshimiwa Mwai Kibaki alisema kutakuwa na free primary education. Watu walimkejeli na wakasema hiyo haiwezekani,” alisema.
Ruto alisisitiza kuwa hakuna mtoto wa Kenya anayepaswa kukosa nafasi ya kusoma kwa sababu ya ukosefu wa karo.
“Mimi nasema mbele yenu leo ya kwamba watoto wetu wa university na wale ambao wanaenda tertiary institutions going forward serikali ya Kenya itakuwa na funding model ya kuhakikisha hawa watoto wote wanapata pesa ya kusoma na hakuna mtoto wa Kenya atakosa nafasi ya kusoma kwa sababu ya mambo ya kukosa pesa,” alisema.
Umati ulishangilia alipohoji, “Mnasema tuendelee ama tuendelee?”
Ruto aliwapuuza wakosoaji wanaodai sera zake hazitekelezeki, akisema anajua anachofanya.
“Na mimi si wazimu. Na mimi si mlevi. Na mimi si mjinga. I know what I am saying,” alisema.
Alitaja miradi ya nyumba za bei nafuu, ujenzi wa masoko na hosteli za vyuo vikuu kama ushahidi kuwa ajenda yake iko sawa.
“Si nilisema tutafanya affordable housing. Inajengwa haijengwi? Inajengwa. Masoko inajengwa haijengwi? Inajengwa. Hostels inajengwa haijengwi? Inajengwa. So I know what I’m doing,” alisema.
