By:Hassan Pojjo

Wananchi wa Wadi ya Jomvu Kuu wamejitokeza kwa wingi kushiriki kikao cha ushirikishwaji wa umma kuhusu upangaji wa miradi ya maendeleo itakayofadhiliwa kupitia Hazina ya Maendeleo ya Maeneo Bunge (NG-CDF) kwa miaka ya kifedha 2026 hadi 2028.
Kikao hicho kilichofanyika katika Ofisi ya Msimamizi wa Wadi ya Jomvu Kuu, kiliwapa wakazi fursa ya kueleza mahitaji yao na kupendekeza miradi wanayoamini itachochea maendeleo ya eneo hilo.
Miongoni mwa vipaumbele vilivyotajwa ni kuboresha sekta za elimu, afya, miundombinu, usalama, pamoja na uwezeshaji wa vijana na wanawake na uimarishaji wa mazingira ya kujifunzia katika taasisi za elimu.
Akizungumza katika mkutano huo, Mbunge wa Jomvu, Badi Twalib, alisema ushirikishwaji wa wananchi ni msingi muhimu wa kuhakikisha fedha za NG-CDF zinaelekezwa katika miradi inayokidhi mahitaji halisi ya jamii.

Alifafanua kuwa zoezi hilo hufanyika kila baada ya miaka miwili ili kuwapa wananchi nafasi ya kuamua vipaumbele vya maendeleo katika maeneo yao, huku akisisitiza kuwa maoni yao yatatumika katika kuandaa mpango wa utekelezaji wa miradi hiyo.
Mbunge huyo aliwapongeza wakazi kwa kujitokeza kwa wingi na kutoa maoni yao kwa uwazi, akisema ushiriki wao unaimarisha uwajibikaji, uwazi na matumizi bora ya fedha za umma.

Naye alisema, “Maendeleo ya kweli yanapatikana pale wananchi wanaposhiriki katika kufanya maamuzi. Maoni yenu ndiyo yatakayoongoza utekelezaji wa miradi yenye manufaa kwa jamii.”
Kwa upande wao, wananchi waliwasilisha mapendekezo mbalimbali yaliyolenga kuboresha huduma za msingi na kuinua hali ya maisha ya wakazi wa Jomvu Kuu, wakieleza matumaini kuwa maoni yao yatazingatiwa katika utekelezaji wa miradi ya NG-CDF kwa kipindi cha miaka miwili ijayo.

Ushirikishwaji huo ni sehemu ya matakwa ya kisheria yanayolenga kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika kupanga na kufuatilia miradi ya maendeleo, hatua inayochangia maendeleo shirikishi na endelevu katika Eneo Bunge la Jomvu.

