Share this to

By:Glory Mwagambo

Wakazi wa Malindi katika Kaunti ya Kilifi wamekemea vikali matumizi ya lugha ya matusi na kejeli miongoni mwa viongozi wa kisiasa wakati huu wa kampeni kuelekea uchaguzi mkuu.

Wakazi hao wamesema viongozi wanapaswa kuwa mifano bora kwa jamii kwa kutumia lugha ya staha na kuwasilisha sera zenye lengo la kuleta maendeleo, badala ya kushambuliana kwa maneno machafu.

Jonathan Nzaro, mkazi wa Malindi, amesema viongozi wanaotumia lugha za matusi wanashusha heshima ya nafasi wanazowania na kuwapa wananchi mfano mbaya.

Nzaro amesema wananchi wanahitaji kusikia mipango ya maendeleo itakayoboresha maisha yao, akisisitiza kuwa siasa inapaswa kuwa jukwaa la kuleta umoja na maendeleo, wala si chanzo cha migawanyiko na chuki.

Amesema hakuna mwananchi atakayevutiwa kumpigia kura kiongozi anayekosa heshima kwa kutumia lugha isiyofaa, huku akitoa wito kwa viongozi kuonyesha ukomavu wa kisiasa.

Kauli hiyo imeungwa mkono na Jacob Wasakina, ambaye amesema ingawa msimu wa uchaguzi mara nyingi huambatana na joto la kisiasa, viongozi hawapaswi kutumia hali hiyo kama kisingizio cha kutoa matamshi ya kudhalilisha wengine.

Wasakina amesema viongozi wanapaswa kuwa waangalifu kwa kuwa mienendo yao inaathiri moja kwa moja vijana na watoto ambao ni viongozi wa kesho.

Aidha, amewataka wananchi kuwa makini na viongozi wanaotumia chuki na propaganda kuwagawa wananchi, akisisitiza umuhimu wa kuchagua viongozi wanaohubiri amani, umoja na maendeleo.


Share this to

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *