By:Menza Ali

Vita dhidi ya dhuluma za kijinsia katika Kaunti ya Kilifi vimepata msukumo mpya kufuatia uzinduzi wa kituo cha uokoaji na hifadhi yaani Safe House, chenye uwezo wa kuhifadhi manusura 48 katika eneo la Kilifi Kaskazini.
Kituo hicho kimejengwa na shirika la Shining Hope for Communities (SHOFCO) kwa ushirikiano na Serikali ya Kaunti ya Kilifi, wakati ambapo visa vya dhuluma dhidi ya wanawake na wasichana vinaendelea kuongezeka katika kaunti hiyo.
Kulingana na takwimu za Baraza la Kitaifa la Utekelezaji wa Haki (NCAJ), kesi za dhuluma za kijinsia zilizowasilishwa mahakamani Kilifi ziliongezeka kutoka visa 939 mwaka wa 2024 hadi visa 1,024 mwaka wa 2025.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Katibu Mkuu katika Wizara ya Jinsia, Anne Wang’ombe, amesema kituo hicho ni hatua muhimu katika kuimarisha ulinzi wa manusura na kuhakikisha wanapata huduma za matibabu, usaidizi wa kisaikolojia na haki.
Naye Naibu Gavana wa Kilifi, Flora Chibule, amesema Kimbilio Safe House ni kituo cha kwanza rasmi cha aina yake katika kaunti hiyo, kilichotengwa mahsusi kwa ajili ya kuwahifadhi manusura wa dhuluma za kijinsia.
Kwa upande wake, mwanzilishi wa SHOFCO, Dkt. Kennedy Odede, amesema kituo hicho kitatoa huduma jumuishi zitakazowasaidia manusura kupona, kujijenga upya na kurejea katika maisha ya kawaida.
