Share this to

Sekta ya uvuvi mjini Malindi, Kaunti ya Kilifi, inaendelea kukumbwa na changamoto kutokana na kupungua kwa idadi ya samaki baharini, hali ambayo imewaathiri mamia ya wavuvi wanaotegemea shughuli hiyo kujipatia riziki.

Wavuvi wanasema mabadiliko ya tabianchi yamechangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa samaki, jambo lililosababisha uzalishaji kushuka na mapato yao kuendelea kudorora.

Kiongozi wa Shirika la Aden International Marine, Alex Sere, amesema changamoto hiyo imeathiri pia biashara ya usafirishaji wa samaki katika masoko ya kimataifa kutokana na kupungua kwa mavuno ya baharini.

Sere amesema ukosefu wa mafunzo ya kisasa kwa wavuvi umechangia kudhoofika kwa sekta hiyo. Ameitaka serikali kuimarisha mafunzo ya uvuvi, kutafuta masoko ya uhakika kwa bidhaa za wavuvi pamoja na kupunguza ada za leseni ili kuwapa nafuu katika kipindi hiki cha changamoto za kiuchumi.

Naye mfanyabiashara wa samaki Yusuf Abdirazak amesema ameshuhudia sekta ya uvuvi ikizorota kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa hapo awali tangu aanze kujihusisha na shughuli hiyo.

Amesema mabadiliko ya tabianchi yameathiri shughuli za uvuvi na kusababisha kupungua kwa mapato ya wavuvi wengi wanaoutegemea kama chanzo kikuu cha kipato.

Yusuf amewahimiza wavuvi kukumbatia mbinu za kisasa za uvuvi ili kuongeza tija na kuhakikisha sekta hiyo inarejea katika hali ya uzalishaji endelevu.


Share this to

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *