By:Hassan Pojjo

Wanafunzi wa shule za Memon Academy ya Mvita, Almiraj Academy ya Likoni na Precious Hope School ya Kitutu Chache, Kaunti ya Kisii, wamepata fursa ya kujifunza kwa vitendo namna sheria zinavyotungwa Bungeni kupitia ziara ya kielimu katika Bunge la Kitaifa.
Katika ziara hiyo, wanafunzi hao pamoja na walimu wao walipokelewa na Mbunge wa Jomvu, Badi Twalib, aliyesema kuwa ziara za aina hiyo zina mchango mkubwa katika kuwajengea vijana uelewa kuhusu utendaji wa taasisi za kidemokrasia nchini.
Badi alisema wanafunzi walipata nafasi ya kushuhudia shughuli za Bunge, kujifunza hatua mbalimbali za utungaji wa sheria, jinsi mijadala ya wabunge inavyoendeshwa na wajibu wa Bunge katika kuisimamia serikali na kuwakilisha wananchi.
Alibainisha kuwa elimu ya uraia ni nguzo muhimu katika kujenga kizazi kinachotambua haki, wajibu na umuhimu wa kushiriki katika maendeleo ya taifa, akisisitiza kuwa vijana wanapaswa kupewa fursa za kujifunza kuhusu uongozi bora wakiwa bado shuleni.
Mbunge huyo pia aliwapongeza walimu wa shule hizo kwa kuandaa ziara hiyo ya kielimu, akisema mbinu za kujifunza nje ya darasa huwapa wanafunzi uzoefu wa moja kwa moja unaowasaidia kuelewa vyema masomo yao.
Aliwahimiza wanafunzi kutumia maarifa waliyoyapata kama msingi wa kuwa viongozi waadilifu na raia wanaowajibika, huku akiahidi kuendelea kuunga mkono programu za elimu zinazowakuza vijana na kuwaandaa kwa majukumu ya uongozi wa baadaye.
Ziara hiyo ilihitimishwa kwa kipindi cha maswali na majibu, ambapo wanafunzi walipata nafasi ya kujadili na Mbunge huyo masuala mbalimbali kuhusu shughuli za Bunge na nafasi ya viongozi katika kuwatumikia wananchi.
