By:Hassan Pojjo

Aliyekuwa Waziri wa Utumishi wa Umma, Aisha Jumwa, ametangaza kujiondoa rasmi katika Chama cha United Democratic Alliance, UDA, hatua inayotarajiwa kuathiri siasa za Pwani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027.
Akizungumza na wanahabari, Jumwa amesema amefikia uamuzi huo baada ya kutafakari kwa kina, kufanya maombi na kushauriana na wananchi anaowahudumia.
Jumwa amesema kuanzia sasa si mwanachama wa UDA, akieleza kuwa atatangaza mwelekeo wake mpya wa kisiasa hivi karibuni.
Amesema amekuwa akikabiliwa na kile alichokitaja kuwa kutengwa na kudhalilishwa kisiasa, licha ya kumuunga mkono Rais William Ruto kwa muda mrefu.
Hata hivyo, Jumwa hakufichua chama atakachojiunga nacho, akisema bado anaendelea na mashauriano kuhusu hatua yake ijayo.
Uamuzi huo unajiri huku shughuli za kisiasa zikizidi kushika kasi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027, na macho sasa yakielekezwa kwenye hatua inayofuata ya mwanasiasa huyo katika siasa za Kilifi na Pwani.
