Share this to

By:Robert Mutasi

Wazee wa jamii ya Wakikuyu katika eneo la Molo, Kaunti ya Nakuru, wametoa wito wa amani na mshikamano miongoni mwa jamii mbalimbali nchini, taifa linapoelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Wakiongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Wakikuyu wa Molo, John Njenga, wazee hao wamesema wamejitolea kushirikiana na wenzao kutoka jamii ya Wakalenjin kuimarisha amani na utulivu katika eneo hilo.

Molo, Kuresoi, Elburgon na Njoro ni miongoni mwa maeneo yenye mchanganyiko mkubwa wa jamii za Wakikuyu na Wakalenjin, ambazo zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu katika biashara, kilimo na shughuli nyingine za kijamii.

Akizungumza Molo Jumanne, Julai 29, 2026, Njenga alisema wazee wana wajibu wa kuongoza juhudi za kuzuia migogoro na kuhakikisha jamii zinaishi kwa amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

Alisema wazee kutoka jamii ya Wakalenjin pia wameonyesha nia ya kushiriki katika mazungumzo ya kujenga amani, akisisitiza umuhimu wa kuendeleza historia ya ushirikiano kati ya jamii hizo.

Kwa upande wake, mkazi wa Elburgon, Joram Kariuki, amewataka wanasiasa kujiepusha na matamshi ya uchochezi na badala yake kuhimiza amani, akisema wakazi wa Nakuru hutegemeana katika biashara, kilimo na shughuli nyingine za kiuchumi.

Wazee hao wameitaka Tume ya Taifa ya Mshikamano na Utangamano, NCIC, serikali ya Kaunti ya Nakuru na vyombo vya usalama kuunga mkono juhudi za amani mashinani na kuchukua hatua dhidi ya wanaochochea chuki.

Wito huo unajiri huku shughuli za kisiasa zikitarajiwa kushika kasi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027, na maeneo yenye historia ya migogoro yakihimizwa kuanza maandalizi ya amani mapema.


Share this to

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *