Share this to

By:Robert Mutasi

Wakulima wa miwa Kusini mwa Nyanza wameitaka serikali kusitisha mara moja uagizaji wa sukari kutoka nje, wakisema hatua hiyo inazidi kudidimiza sekta ya miwa nchini.

Wakulima hao wanasema soko la ndani limejaa sukari ya bei nafuu kutoka mataifa ya kigeni, hali inayosababisha sukari inayozalishwa na viwanda vya humu nchini, ikiwemo Sony Sugar, kukwama maghalani bila kupata wanunuzi.

Kulingana na wakulima, hali hiyo imeathiri uwezo wa viwanda kuwalipa wakulima kwa miwa wanayowasilisha, na kuwaacha wakikabiliwa na changamoto za kifedha.

Mkulima Austine Ouma amesema baadhi yao wamekuwa wakisubiri malipo kwa miezi kadhaa, hali inayowafanya washindwe kugharamia mahitaji ya msingi kama mishahara ya wafanyakazi, karo za watoto na matunzo ya mashamba.

Wakati huohuo, wakulima wameibua wasiwasi kuhusu biashara haramu ya sukari inayokwepa kodi na kuingia sokoni kwa bei ya chini, wakisema inazidisha ushindani usio wa haki kwa wazalishaji wa ndani.

Vitalis Okinda, mkulima kutoka Migori, amehoji ukimya wa viongozi waliochaguliwa huku wakulima wakiendelea kukumbwa na changamoto hizo.

Wakulima hao sasa wanaitaka serikali kuimarisha udhibiti mipakani, kukabiliana na uagizaji haramu wa sukari na kuweka mbele uzalishaji wa ndani ili kulinda viwanda na maisha ya maelfu ya wakulima wa miwa.


Share this to

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *