By:Robert Mutasi

Mahakama Kuu ya Nakuru imemwachilia huru Seneta wa Uasin Gishu Jackson Mandago katika kesi ya ufisadi wa Sh1.1 bilioni za mpango wa masomo ya ughaibuni.
Katika uamuzi uliotolewa Alhamisi, Julai 23, mahakama ilisema upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha mashtaka ya njama ya kuiba na matumizi mabaya ya ofisi dhidi ya aliyekuwa gavana huyo.
Mandago alishtakiwa pamoja na maafisa wawili wa zamani wa kaunti baada ya pesa zilizochangwa na wazazi kwa ajili ya wanafunzi kusomea nje ya nchi, hasa Ufini na Kanada, kudaiwa kupotea.
Mpango huo, uliozinduliwa wakati Mandago akiwa gavana, uliwataka kila mnufaika kuchangia hadi Sh1 milioni kwenye akaunti ya pamoja ya kaunti ili kulipia karo, malazi na usafiri.
Matatizo yalijitokeza Septemba 2021 baada ya wazazi kulalamika kukosa mawasiliano, huku wanafunzi walioko Ufini wakiripoti kufukuzwa kwenye nyumba zao kwa kushindwa kulipa karo. Kaunti iliwajibu kuwa mfuko umeisha na hauwezi tena kuwalipia wanafunzi.
Uchunguzi wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi, EACC, ulibaini wazazi walichanga takriban Sh957 milioni, lakini Sh257 milioni pekee ndizo zilitumika kulipia karo na matumizi mengine. EACC ilidai takriban Sh700 milioni zilitumika vibaya.
Kufichuliwa huko kulizua maandamano Eldoret, na kusababisha Mandago na wenzake kukamatwa Agosti 2023 kwa mashtaka ya njama ya wizi, matumizi mabaya ya mamlaka na kuvunja sheria.
Mahakamani, Mandago alikana kuhusika, akisema mpango huo ulilenga kusaidia wanafunzi wasiojiweza kupata elimu ya kimataifa na changamoto zilitokana na mawakala wa kigeni na kupanda kwa viwango vya ubadilishaji wa pesa.
Mahakama ilisema ushahidi haukutosha kumtia hatiani, na hivyo kumaliza kesi iliyodumu zaidi ya miaka sita.
Uamuzi huo umepokelewa kwa hisia tofauti na wazazi walioathirika, ambao bado wanadai kurejeshewa pesa zao na fidia kwa wanafunzi walioathirika. Upande wa mashtaka umesema utapitia hukumu hiyo kabla ya kuamua kama utakata rufaa.
