Share this to

By:Hassan Pojjo

Mashindano ya Kamoti Junior Super Cup makala ya tatu yanaingia hatua ya robo fainali Jumapili, Julai 26, 2026, huku mechi mbili zikitarajiwa kuwakutanisha baadhi ya timu bora na kuvutia mashabiki kutoka maeneo mbalimbali ya Kaunti ya Kilifi.

Katika mchezo wa kwanza, Red Scorpion FC itamenyana na Young Strikers FC kuanzia saa 9:00 alasiri katika Uwanja wa Mgala. Timu zote mbili zimeonyesha kiwango kizuri tangu kuanza kwa mashindano, hali inayotarajiwa kufanya mchezo huo kuwa wa ushindani mkali huku kila upande ukisaka tiketi ya kutinga nusu fainali.

Mchezo wa pili utawakutanisha Lexcon FC na M’Barakani FC, pia kuanzia saa 9:00 alasiri. Hata hivyo, waandaaji wametangaza mabadiliko ya uwanja, ambapo badala ya kuchezwa katika Uwanja wa Lugwe kama ilivyopangwa awali, sasa mchezo huo utafanyika katika Uwanja wa Shule ya Sekondari ya Rabai.

Kwa mujibu wa waandaaji, mabadiliko hayo yamelazimika kufanywa kutokana na ratiba nyingine ya soka katika Uwanja wa Lugwe, ambapo kutakuwa na mchezo kati ya Usintate FC na Silver Bullet FC, hivyo kuepusha mgongano wa ratiba.

Waandaaji wamewahimiza mashabiki kujitokeza kwa wingi na kufika mapema katika viwanja husika kushuhudia mechi hizo, huku wakidumisha amani na kuzingatia utaratibu wakati wote wa mashindano.

Kamoti Junior Super Cup imeendelea kujijengea sifa kama moja ya mashindano muhimu ya ukuzaji wa vipaji vya soka katika eneo la Rabai na maeneo jirani, ikitoa jukwaa kwa wachezaji chipukizi kuonyesha uwezo wao mbele ya wadau mbalimbali wa mchezo huo.


Share this to

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *