Share this to

By:Hassan Pojjo

Mbunge wa Jomvu, Badi Twalib, ameongoza ziara ya maendeleo katika eneo la Aldina, ambapo alizindua rasmi Barabara ya Aldina Catholic Access Road na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Barabara ya Mzunguko ya Aldina–Makenga (Aldina–Makenga Ring Road).

Akizungumza katika hafla iliyohudhuriwa na mamia ya wakazi, Badi alisema miradi hiyo ni sehemu ya mpango wa kuboresha miundombinu katika eneo bunge la Jomvu ili kurahisisha maisha ya wananchi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

Alisema barabara hizo zitaboresha usafiri na mawasiliano kati ya maeneo mbalimbali, kurahisisha biashara, kuongeza fursa za uwekezaji na kuwawezesha wananchi kufikia kwa urahisi huduma muhimu kama shule, hospitali na masoko.

Mbunge huyo alisisitiza kuwa uwekezaji katika miundombinu ni msingi wa maendeleo endelevu, akiahidi kuendelea kutekeleza miradi zaidi ya maendeleo katika sehemu mbalimbali za Jomvu.

“Ninawashukuru wananchi wa Aldina kwa kuendelea kutuunga mkono. Ushirikiano wenu unatupa nguvu ya kuendelea kusukuma mbele ajenda ya maendeleo ya Jomvu,” alisema.

Badi pia aliwapongeza wakazi kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika ziara hiyo, akieleza kuwa ushirikiano wao ni muhimu katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa mafanikio.

Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na MCA wa Wadi ya Jomvu Kuu, Joshua Ong’au Mose, pamoja na viongozi wengine wa eneo hilo, ambao walieleza kuwa ujenzi wa barabara hizo utarahisisha usafiri, kuunganisha maeneo mbalimbali na kuchochea ukuaji wa shughuli za kijamii na kiuchumi.

Ziara hiyo ilihitimishwa kwa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na viongozi wao ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inakamilika kwa wakati na kuleta manufaa kwa wakazi wote wa Jomvu.


Share this to

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *