By:Glory Mwagambo

Wakazi wa eneo la Kajajini, mjini Malindi katika Kaunti ya Kilifi, wameonyesha furaha na kumpongeza Mbunge wa Malindi, Amina Mnyazi, baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa shule mpya katika eneo hilo.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mnyazi alisema mradi huo unalenga kuimarisha upatikanaji wa elimu kwa watoto wa Kajajini, akisisitiza kuwa elimu ndiyo msingi wa maendeleo ya jamii. Alieleza kuwa katika awamu ya kwanza, shule hiyo itajengwa ikiwa na madarasa manne pamoja na vyoo vya walimu na wanafunzi.

Mbunge huyo alisema watoto wengi wamekuwa wakikosa fursa ya elimu kutokana na umbali wa shule zilizopo, hali inayowalazimu kutembea masafa marefu au kuacha masomo kabisa. Aidha, alisema msongamano mkubwa wa wanafunzi katika madarasa ya shule jirani umekuwa changamoto nyingine inayohitaji suluhisho la haraka.
Mnyazi aliongeza kuwa ujenzi wa shule hiyo utachangia kuimarisha usalama wa watoto kwa kuwapa mazingira bora ya kujifunzia. Pia alisema mradi huo utatoa nafasi za ajira kwa walimu na wakazi wa eneo hilo, huku biashara ndogo ndogo zikitarajiwa kunufaika kutokana na ongezeko la shughuli za kiuchumi.

Aliwahimiza wakazi kushirikiana katika kuutunza na kuukuza mradi huo, akisisitiza kuwa shule hiyo ni mali ya jamii nzima na kwamba wazazi wana jukumu la kuhakikisha watoto wanapata elimu bora.

Kauli yake iliungwa mkono na Mwenyekiti wa shule hiyo, Edward Thoya, aliyemshukuru mbunge kwa kutimiza ahadi ya muda mrefu ya kujenga shule katika eneo hilo. Alisema mradi huo utapunguza mateso ambayo watoto wamekuwa wakiyapitia kwa kutembea umbali mrefu kwenda shule, hali ambayo imekuwa ikichangia baadhi yao kushindwa kuendelea na masomo.

Thoya alisema uwepo wa shule hiyo pia utasaidia kupunguza uhalifu kwa kuwa watoto wengi watakuwa shuleni na kupata maadili pamoja na elimu kuhusu umuhimu wa amani na usalama. Aliongeza kuwa biashara za wakazi zitapata msukumo mpya, huku vijana wa eneo hilo wakipewa kipaumbele katika ajira za ujenzi wa shule.
Aidha, aliwataka viongozi na wazazi kuendelea kuhamasisha watoto kuthamini elimu na kujiepusha na kuzurura mitaani, akisema elimu ndiyo njia bora ya kujenga mustakabali wa jamii.
