
Serikali imeanza kuondoa mfumo wa zamani wa uchunguzi wa uhalifu uliotegemea alama za vidole kwa wino na karatasi, na kuanzisha Mfumo wa Kisasa wa Utambuzi wa Kibiometriki (MBIS) unaolenga kuimarisha usalama na kasi ya utoaji wa huduma.
Akizungumza katika makao makuu ya Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) jijini Nairobi, Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, alisema mfumo huo utarahisisha utambuzi wa watuhumiwa, uhifadhi wa kumbukumbu za uhalifu na ufuatiliaji wa wahalifu kwa kutumia teknolojia ya alama za vidole na utambuzi wa sura.
Mkurugenzi wa DCI, Mohamed Amin, alisema MBIS itaboresha uchunguzi wa kesi ngumu za uhalifu kwa kuongeza kasi na usahihi wa uchakataji wa taarifa za kibiometriki.
Naye Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Renson Ingonga, alisema mfumo huo utarahisisha shughuli za mashtaka kwa kuwezesha kubaini kwa haraka iwapo mtuhumiwa ni mkosaji wa kwanza au amerudia kosa.
