By:Hassan Pojo

Timu ya Coast United Football Academy imepoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Volcano Youth katika mechi ya Ligi ya FKF Mombasa County msimu wa 2025/26.
Licha ya kupoteza mchezo huo, benchi la ufundi la Coast United limesema limefarijika na kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wake chipukizi, wakieleza kuwa walicheza kwa nidhamu, kujituma na ari kubwa kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mchezo.
Uongozi wa timu hiyo umebainisha kuwa kila mechi ni fursa ya kujifunza, kurekebisha makosa na kuendelea kujijenga kwa lengo la kupata mafanikio katika siku zijazo.
Kwa upande wake, Volcano Youth ilitumia vyema nafasi ilizozipata na kufanikiwa kuondoka na ushindi wa mabao 2-0, matokeo yaliyoipa pointi muhimu katika mbio za kuimarisha nafasi yake kwenye msimamo wa ligi.
Coast United imeipongeza Volcano Youth kwa ushindi huo na kuitakia kila la heri katika mechi zake zijazo.
Akizungumza baada ya mchezo huo, kocha mkuu wa Coast United, Said Mung’aro, aliwashukuru wachezaji, benchi la ufundi, wazazi na mashabiki kwa kuendelea kuiunga mkono timu hiyo licha ya matokeo yasiyoridhisha.
Alisema ushirikiano na sapoti yao ndiyo nguvu inayoiwezesha timu kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuboresha kiwango chake.
Aidha, Mung’aro alisisitiza kuwa kichapo hicho hakitawavunja moyo, bali kitakuwa somo muhimu litakalowasaidia kurekebisha mapungufu na kurejea wakiwa imara zaidi katika mechi zijazo.
Coast United imeahidi kuendelea kudumisha umoja, nidhamu na kujituma huku ikiendeleza dhamira yake ya kukuza vipaji vya soka miongoni mwa vijana katika Kaunti ya Mombasa.
