By:Glory Mwagambo

Wafanyabiashara wa Soko la Kwa Jiwa mjini Malindi, Kaunti ya Kilifi, wameeleza kufurahishwa na kuimarika kwa biashara zao ikilinganishwa na miaka ya awali, ambapo walikuwa wakikumbwa na mapato duni.
Mwenyekiti wa soko hilo, Safari Mwambire, amesema biashara zimeimarika kwa kiwango kikubwa, jambo ambalo limechangia ongezeko la mapato kwa wafanyabiashara. Amebainisha kuwa shughuli za biashara huchangamka zaidi wakati wa msimu wa watalii, ambapo idadi ya wateja huongezeka.

Aidha, Mwambire amewahimiza vijana wanaozurura mitaani kujitosa katika shughuli za biashara ili kujipatia ajira na kuboresha maisha yao.
Hata hivyo, amesema wafanyabiashara hao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo kuzorota kwa hali ya usafi sokoni kutokana na uhaba wa wafanyakazi wanaosimamia usafi. Amesema hali hiyo huwafanya baadhi ya wateja kukwepa soko kwa kuhofia afya zao, jambo linalopunguza mauzo.

Vilevile, ameeleza kuwa mitaro ya kupitisha maji taka imekuwa kero kubwa kwa wafanyabiashara, kwani huathiri mazingira ya biashara na kuhatarisha afya zao.
Kwa upande mwingine, wafanyabiashara hao wamezitaka serikali na viongozi mbalimbali kuhamasisha zaidi sekta ya utalii ili kuongeza idadi ya wageni wanaotembelea eneo hilo. Pia wameomba kuwepo kwa mikopo nafuu kwa wafanyabiashara wenye kipato cha chini ili kuwawezesha kukuza biashara zao na kuboresha hali yao ya kiuchumi.
