By:Anne Nyakole

Viongozi wa Vyama vya Usimamizi wa Fukwe (BMU) kutoka Kaunti ya Mombasa wanashiriki mafunzo ya siku tatu yanayolenga kuimarisha uwezo wao katika utetezi wa sekta ya uvuvi, uongozi, pamoja na uelewa wa sera na sheria zinazosimamia shughuli za uvuvi nchini.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Naibu Mkurugenzi wa Uvuvi katika Huduma ya Uvuvi Kenya, Benedict Kiilu, amesema mafunzo hayo yatawapa viongozi wa BMU maarifa na ujuzi wa kusimamia rasilimali za uvuvi kwa njia endelevu ili sekta hiyo iendelee kunufaisha kizazi cha sasa na kijacho.
Kiilu amesema viongozi wa BMU ni kiungo muhimu kati ya serikali na jamii za wavuvi, hivyo kuwajengea uwezo kutaimarisha utekelezaji wa sheria za uvuvi, kuongeza ushirikiano na wadau mbalimbali, na kuhamasisha matumizi endelevu ya rasilimali za baharini.

Naye Doreen Simiyu kutoka shirika la Community Action for Nature Conservation (CANCO), ambalo linaandaa mafunzo hayo, amesema lengo ni kuwawezesha viongozi wa BMU kutetea maslahi ya wanachama wao kwa ufanisi huku wakizingatia sera na sheria zinazosimamia sekta ya uvuvi.
Simiyu amesema viongozi wenye uelewa wa kutosha kuhusu mfumo wa kisheria na sera za uvuvi wana nafasi nzuri zaidi ya kushiriki katika maamuzi yanayohusu usimamizi wa rasilimali za baharini na kuchangia maendeleo ya jamii za wavuvi.

