
Sekta ya ujenzi na miundombinu katika Kaunti ya Mombasa imepata msukumo mpya baada ya kuzinduliwa rasmi kwa mafunzo ya ujuzi kupitia mfumo wa PropelA, unaolenga kuwapa vijana stadi zinazohitajika katika soko la ajira.
Mpango huo unalenga kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira na kuziba pengo la ujuzi miongoni mwa vijana kwa kuwaandaa kwa mahitaji halisi ya sekta ya ujenzi na viwanda.

Uzinduzi huo uliwaleta pamoja wadau mbalimbali, wakiwemo Mamlaka ya Kitaifa ya Mafunzo ya Viwandani (NITA) Mombasa na shirika la Swisscontact. Ilielezwa kuwa mafunzo hayo yataendeshwa kwa mfumo wa asilimia 75 ya muda kutumika katika maeneo ya kazi, huku asilimia 25 ikifanyika darasani.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Meneja wa Miradi wa Swisscontact, Jimmy Deylon, alisema mfumo wa PropelA unalenga kuondoa pengo lililopo kati ya elimu na mahitaji ya soko la ajira kwa kuhakikisha wahitimu wanapata ujuzi unaohitajika na waajiri.

Deylon alibainisha kuwa baada ya mpango huo kufanikiwa jijini Nairobi kwa kuwawezesha takriban asilimia 80 ya wahitimu kupata ajira, tayari pia umetekelezwa katika Kaunti ya Kilifi. Sasa Mombasa inatarajiwa kunufaika kupitia mafunzo katika fani za mabomba, ufundi wa nyaya za umeme na teknolojia ya nishati mbadala.

Kwa mujibu wa takwimu zilizowasilishwa wakati wa uzinduzi huo, licha ya sekta ya ujenzi nchini kuwa na thamani ya zaidi ya shilingi trilioni mbili, bado kuna uhaba mkubwa wa mafundi stadi, hali inayochangia pengo kati ya mahitaji ya soko la ajira na idadi ya wataalamu waliopo.

